Maji huitaji mvugulio!

Thursday, February 15, 2007

MAKUU
Japo sina wajukuu, ninao mkubwa umri,
Nashukuru alo juu, yeye mwingi wa mazuri,
Manju navunja kifuu, kwa kulitunga shairi,
Nafuu sina makuu।

Hii kwangu ni nafuu, namshukuru Rasuri,
Wenye kupenda makuu, mwisho wao simzuri,
Wengi huvunjoika guu, mmeyaona tayari,
Nafuu sina makuu।

Sasa hata vitukuu, mambo yao sharishari,
Kama walaji tamnbuu, mambo yao ya hatari,
Elimu yao juzuu, wanaitia shubiri,
Nafuu sina makuu।


Mmeyaona tayari, mwenye makuu hadumu,
Huyataka ya fahari, kwa ulafi wa matamu,
Pesa ni wao urari, japo kwao ni adimu,
Nafuu sina makuu।

Wao wanajivinjari, mamnane yakishatimu,
Magwanda ya askari, huvaa wakahujumu,
Usoni mithili Ngiri, kuua ni yao hamu,
Nafuu sina makuu।

Nondo hata misumari, silaha zao muhimu,
Hawaogopi kaburi, ama kuua kaumu,
Ama dhambi mas'huri, kwakuwa huvuta ndumu,
Nafuu sina makuu।

Atavuka na bahari, kama asiye timamu,
Akiukosa urari, yu tayari kunywa sumu,
Ama kuifanya shari, watu awamwage damu,
Nafuu sina makuu।

Watu awamwage damu, apate kiti cha enzi,
Utamshinda ugumu, hata kwamambo ya penzi,
Akimkosa Swaumu, atajitia kitanzi,
Nafuu sina makuu।

Shairi hili salamu, kwa wenye tabia hizi,
Wenye akili timamu, wanojitia uchizi,
Maisha siyo rehamu, ninyi mnayatatizi,
Nafuu sina makuu।

Jifunzeni mfahamu, kaditama ya ujenzi,
Mambo yake fumufumu, rafiki zake ni nzi,
Bado sijaisha hamu, kesho nitawapa tenzi
Nafuu sina makuu।